Facebook,
mitandao mingine ya kijamii pamoja na huduma ya ‘blackberry mesenger’
maarufu kama BBM huathiri watu kisaikolojia, husababisha ndoa kuvunjika
pamoja na usaliti katika uhusiano, wanasayansi wamebaini.
Utafiti
huo uliofanywa mwaka 2012 na wanasayansi wa nchini Israel umebaini kuwa
kwa wastani, wanawake wanatumia dakika 81 katika mitandao ya kijamii kwa
siku ukilinganisha na wanaume ambao hutumia dakika 64, huku watu wasio
na elimu wakionekana kuathirika zaidi na mitandao hiyo.
Watafiti
hao kutoka Chuo Kikuu cha Tel Aviv walihusisha matukio kadhaa ya
kisaikolojia kati ya watu walioathirika na mtandao na udanganyifu
uliosababishwa na uhusiano unayoanzishwa kupitia mitandao ya kijamii.
Utafiti
huo ulibaini kuwa wote waliohusishwa walikuwa na tatizo la upweke,
ingawa hakuna aliyekuwa na historia ya matumizi ya dawa za kulevya au
matatizo ya kisaikolojia.
Watu
wenye upweke walionekana kupendelea kutafuta uhusiano kupitia mitandao,
jambo linaloelezwa kusababisha kuwaumiza watu hao na kuhisi kusalitiwa.
Kiongozi
wa utafiti huo Dk Uri Nitzan kutoka Chuo Kikuu cha Sackler mchepuo wa
Tiba na Afya ya Akili, Shalvata Mental Health Care Centre alisema: “Kama
ilivyo matumizi ya mtandao yanazidi kuwa makubwa. Vivyo hivyo
inavyozidi kuhusiana na masuala ya saikolojia. Mawasiliano ya kompyuta
kama Facebook na makundi ya mawasiliano yaliyopo ndani ni sehemu muhimu
ya habari hii.”
Utafiti
huo awali ulihusisha wagonjwa watatu ambapo Dk Nitzan anasema kuwa
utafiti wao ulibaini kuwapo na mawasiliano kati ya saikolojia za
wagonjwa hao na mawasiliano ya mitandao ikiwemo Facebook. Dk Nitzan
anasema kuwa wagonjwa wote watatu waliachana na maisha ya upweke na
kupata furaha baada ya kupata wapenzi wapya kupitia mitandao.
Anasema: “Ingawa
uhusiano wau huwa na mtazamo chanya awali, lakini huishia kuwa na
mawazo ya kuumizwa, kusalitiwa na uvamizi wa faragha. Watu hawa
walibadilishana mawazo, ikiwamo upweke na mazingira magumu katika hasira
au kutengana na watu waliowapenda awali, kutokana na teknolojia
hawakuwa na historia ya kunyanyaswa,” anasema na kuongeza:
“Katika
kila kesi, kulikuwa na uhusiano baina ya kuwapo na maendeleo ya taratibu
na ongezeko la dalili za kuathirika kisaikolojia, pamoja na
udanganyifu, wasiwasi, kuchanganyikiwa na matumizi yaliyozidi ya
mawasiliano ya kompyuta.
”Dk
Nitzan anasema kuwa tatizo kubwa la mitandao ni watu kuanzisha uhusiano
kabla ya kuonana ana kwa ana, tatizo ambalo husababisha mtu kumwona
mwenzake anamfaa, huku hali ikiwa ni tofauti pindi wawili hao
wanapokutana. Aliongeza kuwa wataalamu wa afya ya akili lazima waache
ushawishi wa matumizi ya mitandao ya kijamii wanapozungumza na wagonjwa.
“Unapowauliza
watu kuhusu maisha yao ya kijamii ni busara zaidi kuwauliza juu ya
matumizi ya Facebook na mitandao mingine ya kijamii, kama matumizi ya
mitandao,”anasema.
Anaongeza: “Utafiti
wetu unaonyesha, wakati teknolojia kama Facebook ikiwa na faida nyingi,
baadhi ya watu wamekuwa wakiathirika na mitandao hii ya kijamii, huku
ikiwavutia walio wapweke au walio katika mazingira magumu katika maisha
yao ya kila siku, wakati wengine wakilazimisha tabia zisizo zao.”
Wataalamu Dar
Mwanasaikolojia
na Mkurugenzi wa Kliniki ya NEHOTA inayotoa huduma ya ushauri iliyopo
Makongo Juu jijini, Dk Bonaventura Mutayoba Balige anasema kuwa tatizo
kubwa linalowafanya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuathirika
kisaikolojia ni uhusiano unayoanzishwa kupitia mitandao hiyo. Uhusiano
unaoanzishwa katika mitandao ya kijamii hata ukiwa na matokeo chanya na
kuanzisha ndoa, mara nyingi wanandoa hao huhisi kuumizwa au kusalitiwa
muda wowote, jambo linalosababisha migogoro ya mara kwa mara.
“Unapokuwa
na mume au mke mliyekutana Facebook, kisha akaendelea kutumia mtandao
huo, bila shaka anapokuwa bize mtandaoni muda mwingi, mwenzake huanza
kuathirika kisaikolojia kwani huanza kuumia kwa kuhisi kusalitiwa na
mweza wake,” anasema mwanasaikolojia huyo.
Dk Balige
anasema kuwa licha ya kuwepo watu wanaoathirika kwa kuwa mitandaoni
muda wote, bado idadi ya watu wanaoanzisha uhusiano kwenye mitandao hiyo
wakiwa kwenye hatari ya kuathirika zaidi, hasa kutokana na udanganyifu
uliopo.
“Picha
hazisemi kweli; wapo watu wakipiga picha haitoki kama alivyo. Hivyo
mwanamke au mwanamume akianzisha uhusiano kwa kutegemea picha aliyoiona
Facebook, bila shaka anaweza asitamani kuendelea na uhusiano huo
atakapokutana na mtu husika ana kwa ana,” anasema Dr Balige.
Tafiti nyingine
Machi
8, 2011 wanasheria nchini Marekani walitoa ripoti yao kuwa mtandao wa
Facebook ni chanzo cha migogoro katika uhusiano. Pia husababisha ndoa
nyingi kuvunjika, hali inayosababisha kuongezeka kwa kesi za kudai
talaka mahakamani.
Wanasheria
hao walisema chanzo cha talaka nyingi ni mtandao wa Facebook ikiwamo
‘Blackberry messenger’ (BBM), huku ‘My Space’ ikichangia kwa asilimia 15
na Twitter kwa asilimia 5.
Mwanasaikolojia
na mshauri wa ndoa kutoka Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Loyola, Chicago
Dk Steven Kimmons amewahi kusema: “Nimepokea kesi nyingi, mojawapo ni
mwanamume aliyekutana na mwanamke aliyesoma naye kwenye mtandao wa
Facebook na kuanza uhusiano, huku akiwa ameshaoa. Ni tatizo kubwa.”
Mikasa ya Facebook
Kijana
mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Henry anasema kuwa aliwahi
kufungua akaunti ya Facebook na barua pepe feki vyote vikiwa na jina la
msichana. Aliombwa urafiki na wanaume wengi, ambao walimtongoza na
baadaye aliamua kumkubali mmoja aliyemfahamu, akiwa pia mtu wake wa
karibu bila mtu huyo kumgundua.
“Nilianza
kuchati naye, alinipenda kupitia picha niliyoiweka kwenye ukurasa
wangu. Alinitumia barua pepe pia, baada ya miezi miwili alihitaji
kuniona niliamua kufunga akaunti hiyo baadaye,” anasema Henry
aliyebainisha kuwa mwanaume huyo alikuwa ni mume wa mtu.
Rahel
Simon (si jina lake halisi) anasema kuwa alikutana na mume wake mwaka
2009 kwenye mtandao wa Facebook. Walipendana na kwa kuwa wote waliishi
jijini Dar es Salaam ilikuwa rahisi kuonana.
“Wakati
huo mtandao ulikuwa hauna watu wengi kama ilivyo sasa. Tulijuana na
kufunga ndoa, ila nina wasiwasi wa kusalitiwa, muda mwingi mume wangu
anapokuwa akichati na marafiki zake kupitia mtandao huo. Yaani kuna
wakati huwa najilaumu na kutamani kama tungekutana kanisani, huwa nahisi
kama alivyokutana na mimi ipo siku ataisaliti ndoa,” anasema Rahel.
Mwingine aliyejitaja kwa jina moja la Janet anasema: “Sitaki kusikia uhusiano wa kwenye mtandao.
Nilikutana
na wanaume kadhaa, nikajiingiza katika uhusiano nao, baada ya kunitumia
waliniacha, sidhani kama kuna mwanamume aliye tayari na mwanamke
anayekutana naye kwenye hii mitandao ni waharibifu tu,” anasema kwa jazba.
Mwathirika
mwingine (Hamis) aliyekuwa akitafuta mchumba kupitia Facebook anasema
kuwa alikutana na msichana mmoja kupitia mtandao huo baada ya kuona
picha alizoweka binti huyo kwenye ukurasa wake, zikiwa na staili
mbalimbali na kumpenda, akamtongoza na wakakubaliana kuonana. “Tulipanga
kuonana Ukonga jijini Dar es Salaam. Wakati wote tuliwasiliana kupitia
simu. Aliniambia angefika kwa usafiri wa daladala nilimsubiri kituoni.
Alipofika
alinipigia simu, nilimuuliza umevaaje akaniambia nguo za kitenge.
Nilitupa jicho ila nilipomwona sikuamini, nilizima simu kwa kuwa alikuwa
mbali ili asijue kama ni mimi na kutokomea. Alikuwa ni tofauti na
nilivyomwona Facebook alikuwa mbaya,” anasema Hamis.
Dondoo muhimu
Utafiti
uliofanywa na Chuo Kikuu cha Gothenberg uligundua kwamba watu wenye
kipato cha chini na wenye elimu ndogo wanatumia muda mwingi katika
mtandao wa Facebook.
Katika
kundi hili, wengi wanaotumia muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii
hawana furaha na wametawaliwa hali ya chini katika maisha yao.
Utafiti
unaonyesha zaidi ya asilimia 85 ya watumiaji wa Facebook huingia katika
mitandao hiyo kila siku. Asilimia 26 ya kundi hilo huona ni jambo la
kawaida kwa wao kutoingia mara kwa mara.

No comments:
Post a Comment